Kwa mujibu wa uanishaji uliofanywa na wataalamu wa Shirika la Afya
Duniani yaani WHO, kuna hatua kuu nne za ugonjwa wa VVU/UKIMWI ambazo
ni:
1. Hatua ya kwanza au maambukizi ya mwanzo ya HIV. Hatua hii huwa ni
ya muda wa wiki nne na ni asilimia 20 tu ya watu wenye maambukizi ya VVU
walio kwenye hatua hii ambao hupata dalili na viashiria vikali vya
ugonjwa huu, lakini mara nyingi madaktari hushindwa kutambua kama
mgonjwa amepata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na dalili na
viashiria vyake kufanana sana na dalili za magonjwa mengine. Mgonjwa
aliye katika hatua hii ya kwanza ya maambukizi ya VVU huweza kuonesha
dalili na viashiria kama vile kuvimba tezi, kupatwa na homa kali, kuumwa
koo, kujihisi mchovu, kujihisi maumivu sehemu mbalimbali mwilini
kutokwa na vipele mwilini,kutapika, kuharisha au kuumwa tumbo. Mgonjwa
anayepata dalili na viashiria hivi tunasema kwamba amepata "Acute HIV
infection/Acute HIV retroviral infection au seroconversion illness."
Dalili hizi hutokana na mwili wa mtu mwenye maambukizi ya VVU kuanza
kutengeneza kinga dhidhi ya VVU.
2.Hatua ya Pili ni isiyokuwa na dalili au Clinically Asymptomatic Stage.
Katika hatua hii ambayo inaweza kudumu kwa muda wa miaka 10, mgonjwa
haoneshi dalili au viashiria vyovyote vile isipokuwa anaweza kuwa na
tezi zilizovimba. Kiwango cha VVU kwenye damu hupungua sana lakini
mgonjwa anaweza kuambukiza mtu mwingine yoyote na vipimo vya Ukimwi vina
uwezo wa kutambua uwepo wa maambukizi ya VVU katika damu. Tafiti
mbalimbali zimeonesha kwamba, VVU katika mwili huwa bado vinazaliana na
hukimbilia na hujificha kwenye tezi. Kutokana na kujificha kwake katika
hatua hii, kipimo cha kupima wingi wa virusi vya ukimwi au Viral load
test katika mwili hutumiwa sana ili kuweza kutambua uwepo wa VVU. Kipimo
hiki pia husaidia katika kumpangia mgonjwa tiba yake.
3. Hatua ya Tatu yenye viashiria au Symptomatic HIV infection. Katika
hatua hii kutokana na kuongezeka kwa wingi VVU katika mwili, kinga ya
mwili huzidi kudhoofika suala linalosababisha mambo kadhaa. Kwanza ni
tezi na tishu zilizoathiriwa na VVU huharibika kutokana na maambukizi ya
muda mrefu. Pili VVU hubadilika badilika na kuwa na uwezo zaidi wa
kuathiri tishu na sehemu mbalimbali za mwili na hata kuziua au kuharibu
seli zinazokinga mwili kutokana na maambukizi, zinazojulikana kama T
helper cell, seli T saidizi. Pia mwili hushindwa kumudu uharibifu wa
seli T saidizi na kushindwa kuzalisha seli nyingine mpya.
&&&&&&&&&
Dawa za kufubaisha virusi vya Ukimwi au ARV huanza kutumiwa wakati
seli aina ya CD4 zinapopungua na kufikia kiwango cha chini sana.
Kupungua kwa seli hizi za CD4 ni kielelezo kwamba kinga ya mwili imekuwa
dhaifu. Matumizi ya dawa hizi huboresha kinga ya mwili na kumfanya
mgonjwa kuishi kwa muda mrefu bila kuonesha dalili au viashiria vyovyote
vile, yaani kumrudisha mgonjwa katika hatua ya pili ambayo mwili huwa
hauoneshi dalili za maambukizi. Kama mgonjwa wa VVU hatumii dawa za
kufubaisha VVU au anatumia ARV's ambazo hazimsaidii au hazifanyi kazi
vyema mwilini mwake, basi huendelea kuingia kwenye hatua ya nne ya
Ukosefu wa Kinga Mwili (Ukimwi) au AIDS. Kama nilivyoeleza huko nyuma,
hatua hii hujulikani kama Ukosefu wa Kinga Mwilini [UKIMWI] au AIDS,
ambapo mgonjwa hupata maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na
saratani za aina mbalimbali kutokana na kupungua kwa kinga mwilini.
Vigezo vilivyopangwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuweza
kutambua kama mgonjwa yupo kwenye hatua hii ya UKIMWI hutofautiana kati
ya watu wakubwa na watoto chini ya miaka 5. Pamoja na kuwa WHO wameweka
vigezo vya pamoja, utambuzi wa hatua za ugonjwa wa UKIMWI hutofautiana
kati ya nchi na nchi, kutokana na miongozo tofauti ya nchi hizo. Kwa
watu wazima na watoto walio na umri zaidi ya miaka mitano, uwepo wa
ugonjwa wowote nyemelezi pamoja na kushuka kiwango cha CD4 chini ya 200
mm3 au kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 15 hutambulika kama
ugonjwa wa UKIMWI. Kwa watoto walio chini ya miaka mitano, uwepo wa
ugonjwa wowote nyemelezi au kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 20
kwa wale wenye umri kati ya miezi 12-35 hutambulika kama wana ugonjwa
wa UKIMWI. Watoto wenye umri chini ya miezi 12, kupungua kwa seli za CD4
chini ya asilimia 25 ndiyo hutumika kutambulisha wana ugonjwa wa
UKIMWI. Lakini hebu sasa tueleze CD4 ni nini?
CD4 ni aina ya protini inayopatikana katika ukuta wa seli
zinazojulikana kama seli T saidizi. VVU hushambulia na kujishikiza
kwenye protini hii kabla ya kupata uwezo wa kuathiri seli T saidizi.
Seli hizi za T helper ndizo hulinda mwili dhidi ya maambukizi mbalimbali
na hivyo kuchangia katika kustawi kwa kinga ya mwili. Kupungua kwa seli
hizi mwilini husababisha kupungua kwa kinga ya mwili na hivyo mtu
kupata magonjwa mbalimbali.
&&&&&&&&&&&&&&&&
Baadhi ya magonjwa nyemelezi yanayoweza kumpata mtu mwenye ugonjwa VVU/UKIMWI ni pamoja na
1.Magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vileugonjwa wa homa ya mapafu, kifua kikuu (TB) na saratani aina ya Kaposi's sarcoma.
2. Magonjwa ya mfumo wa chakula kama vile Cryptosporidiosis, fangasi za Candida, Cytomegolavirus (CMV) na Isosporiasis.
3. Magonjwa ya mfumo wa fahamu kama vile Cytomegolavirus,
Toxoplasmosis, Cryptococcosis, saratani aina ya Non Hodgkin's lymphoma,
Varicella Zoster ugonjwa unaojulikana kama mkanda wa jeshi na Herpes
simplex.
4. Magonjwa mbalimbali ya ngozi kama vile Herpes simplex, Kaposi's
sarcoma (saratani ya ngozi) na Varicella Zoster (mkanda wa jeshi].
Kutokana na uhaba wa vifaa vya kupimia kiwango cha seli aina ya CD4
katika nchi mbalimbali, Shirika la Afya Duniani WHO limetengeza mwongozo
mwingine ambao utamsaidia mhudumu wa afya kuweza kutambua kama mgonjwa
amefikia hatua gani ya ugonjwa wa UKIMWI na anastahili kuanza tiba au
la. Uainishaji wa namna hii huitwa clinical classification of HIV/AIDS.
Hatua ya kwanza katika uainishaji huo ni: Mgonjwa hana dalili zozote,
kuwepo kwa uvimbe katika tezi ambao hauondoki au hubakia muda mrefu.
Hatua ya pili ya uainishaji wa hatua ya maambukizo ya Ukimwi
ni, kupungua uzito chini ya asilimia 10 ya uzito wa mwili bila sababu
maalumu, magonjwa ya mara kwa mara kwenye mfumo wa upumuaji kama
magonjwa ya masikio, kinywa, tezi la koo na kadhalika na mkanda wa
jeshi.
Dalili nyingine anazokuwa nazo mgonjwa wa Ukimwi anapokuwa kwenye
hatua hii ni kuwa na vidonda pembezoni mwa mdomo, vidonda vya mara kwa
mara kwenye kinywa, vipele mwilini, ugonjwa wa ngozi na maambukizi ya
fangasi katika kucha.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
Viashiria na dalili zinazoainisha kwamba mgonjwa aliyeambukizwa Ukimwi yupo katika hatua ya tatu au Clinical stage III, ni
• Kupungua uzito kwa zaidi ya asilimia 10 ya uzito wa mwili bila sababu yoyote maalumu.
• Kuharisha zaidi ya mwezi mmoja bila sababu yoyote maalumu
• Kuwa na homa isiyoelezeka [homa hii inaweza kuwa inapona na kujirudia au homa ambayo inakuwepo kwa zaidi ya mwezi mmoja]
• Maambukizi ya fangasi kwenye kinywa [Persistent oral candiadiasis]
• Oral hairy leukoplakia
• Ugonjwa wa kifua kikuu kwenye mapafu [kwenye mapafu]
• Maambukizi hatari ya vimelea vya bakteria [homa ya mapafu, ugonjwa
wa uti wa mgongo, maambukizi katika mifupa na jointi, empyema,
pyomyositis, bacteraemia]
• Maambukizi hatari kwenye kinywa [Acute necrotizing ulcerative stomatitis, gingivitis or periodontitis]
• Upungufu wa damu mwilini bila sababu yoyote maalumu [Unexplained
anaemia (below 8 g/dl), neutropenia (below 0.5 billion/l) and/or chronic
thrombocytopenia (below 50 billion/l)
XXXXXX
No comments :
Post a Comment