Tabora/Manyoni/Dar.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa jana alizua sintofahamu baada ya
kusema; “CCM oyee”, kauli iliyowafanya wananchi hao kukaa kimya na
walipoona akicheka waliitikia “oyeee” huku nao wakicheka na
kumshangilia.
Ingawa ilitokana na ulimi kuteleza, yeye mwenyewe alisema alitamka neno
CCM kama utani ili kubaini ni wananchi wangapi wanaokishabikia chama
hicho kati ya waliojitokeza uwanjani hapo kumsikiliza wakati tayari
amekwishaeleza jinsi chama hicho tawala kilivyoshindwa kuliletea taifa
maendeleo.
Msindai kama Lowassa
Wakati Lowassa akieleza kwamba alisema hayo kwa utani aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai aliyekihama chama hicho
na kujiunga na Chadema, alitoa mpya baada ya kukiombea kura chama chake
hicho cha zamani badala ya Ukawa kwenye mkutano wa hadhara.
Msindai alitoa mpya hiyo juzi jioni wakati akizungumza kwenye mkutano wa
uzinduzi wa kampeni Jimbo la Manyoni Magharibi na Mashariki uliofanyika
Manyoni mjini kwa tiketi ya Ukawa.
Baada ya kuwanadi wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani wa majimbo
hayo, Msindai ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM
Tanzania, aliwaomba wakazi wa Manyoni akisema:
“Mpeni kura Lowassa ni mchapakazi na mwadilifu, anauchukia umaskini
ataikomboa nchi yetu na kura zote za Rais, wabunge na madiwani wapeni
wagombea wa Chama cha Mapinduzi.”
Baada ya tamko hilo, uwanja ulilipuka kwa kelele na minong’ono ndipo
kiongozi mmoja aliponyanyuka na kwenda alipokuwa Msindai ameketi na ni
kama alimwambia: “Hapa ni Ukawa si CCM.”
Alipopata maelekezo hayo, Msindai alisimama na kusema: “Ninaomba radhi,
unajua koo limekauka, hebu kwanza naomba mnipe maji nipooze koo.”
Alipoletewa maji na kuyanywa, aliendelea kuomba radhi na kusema: “Ndugu
zangu, ulimi uliteleza... si mnajua tumetoka huko hivi karibuni Uccm
haujatutoka sawasawa,” alisema na kuamsha kicheko kwa mashabiki
waliokuwa wakimsikiliza.
Akizungumza kwa simu jana, Msindai alikiri kuombea kura wagombea wa CCM
kwenye mkutano wa Ukawa lakini alisema kuwa ulimi uliteleza na kwamba
aliomba radhi na watu walimwelewa.
Hata hivyo, Msindai alikazia kusema kuwa Watanzania wanataka mabadiliko
kwani hata mgombea wa CCM, Dk John Magufuli katika hotuba zake amekuwa
akisema anataka kuona Tanzania ikibadilika.
“Watanzania watabadilika ikiwa Dk Magufuli atatimua watu wote kwenye
mfumo wa utawala na kuleta mabadiliko ya kweli, lakini kama watu
watabakia walewale, watamwangusha,” alisema Msindai.
Alipoulizwa utayari wa Watanzania kubadilika, Msindai alisema Ukawa
ndiyo watakaoleta mabadiliko ya kweli kwa kuwa watawaondosha watu wote
na kuleta watu wapya kwa ajili ya kufanya kazi,” alisema.
Alisema CCM ya sasa siyo ile ya (Julius) Nyerere na imebadilika na
haitumikii tena wananchi na kwamba, Dk Magufuli ni mwenye hasira hivyo
anakosa sifa.
Mmoja wa makada wa Chadema Mkoa wa Singida, Paschal Mlaki alieleza
kushangazwa na kuteleza kwa Msindai akisema ana wasiwasi na waliokuja
kwenye chama hicho. “Mimi ni kada wa Chadema hapa Singida, hakuna
asiyenijua, ukweli hili limetukwaza wengi... hivi inaingia akilini kweli
uko mkutano wa Ukawa ukatangaza CCM?
“Watu wanatumia gharama zao kufanya maandalizi, wanataka kupata vitu vya Ukawa halafu anakuja kututangazia haya!”
Chanzo: Mwananchi
No comments :
Post a Comment