Mtume Petro alimuuliza Yesu Kristo swali hili miaka
elfu mbili iliyopita. “Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia” (Mathayo 24:3).
Katika kulijibu swali hili, Yesu hakutaja mwaka, siku wala saa, badala
yake alielezea dalili zitakazotokea kabla ya siku hii kuu ya kurudi
kwake.
Wasomi wa Biblia wamegundua kwamba
katika kila aya thelathini katika Biblia takatifu, aya moja inazungumzia
juu ya kurudi kwa Yesu. Kinachoonekana hapa ni kuwa kurudi kwake
kumeelezewa mara nyingi zaidi kuliko kuja kwake kwa mara ya kwanza.
Katika Agano la Kale kurudi kwa Bwana kunatajwa mara kwa mara katika
vitabu vya manabii, na katika Agano Jipya ziko sura maalum
zinazozungumzia swala hili. Katika Biblia tunasoma haya: “Huyu
Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo
hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Matendo ya Mitume 1:11).
Unabii huu ndio ujumbe mkubwa katika nabii za Mungu, na ni ukweli
unaogusa mioyo ya wanadamu wote na kuwaletea matumaini wakati wa
mashaka, na kukosa raha. Swali kubwa tunaloweza kujiuliza kuhusiana na
unabii huu wa kurudi kwa Yesu, ni hili la ni lini tukio hili
litakapotokea? Mkristo wa kweli anayefahamu Neno la Mungu hatathubutu
kubashiri saa, siku au mwaka ambao mwisho wa dunia na hukumu ya mwisho
vitatokea. Ufunuo pekee tulio nao ni maneno yaliyotamkwa na Yesu pale
aliposema kuwa, “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe” (Matendo ya Mitume 1:7). Hata
hivyo kutokana na umuhimu wa mambo haya kwa kila wanadamu, Yesu Kristo
hakuwaacha wanafunzi wake katika giza kuhusu siku hii ya hukumu na ya
kurudi kwake. Katika Biblia tunasoma juu ya hali na matukio mbalimbali
yatakayotokea duniani yanayojulikana katika Biblia kama dalili za siku
mwisho.
1)Kutokea kwa nyakati za dhiki
Miongoni mwa dalili za siku za mwisho ni pamoja na vita, kuongezeka kwa
maasi, magonjwa, njaa, matetemeko ya ardhi,ukatili, chuki, kuporomoka
kwa maadili, uzushi, uongo, kutawaliwa na pesa, ukaidi, kuharibu mimba,
kutowajali wengine, ugaidi, tawala mbaya na maovu mengine yanayofanana
na haya
2)Dalili kupotoka kwa wanadamu kiroho
Yesu alitabiri pia kuhusu mafundisho ya uongo pamoja na walimu
watakaopotosha mafundisho ya kweli ya Yesu Kristo. Wakati huo huo
alitabiri kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya wanafunzi wa kweli wa
Yesu Kristo. Biblia imeeleza bayana kuwa wakristo watateswa katika nchi
mbalimbali. Siku hizi tunashuhudia jinsi watu wanavyopotoshwa kiroho kwa
njia mbalimbali. Leo hii kuna dini zinazoshughulikia imani za siri
zinazomkataa Mungu huku kukiwa na ongezeko kubwa la watu wanaojihusisha
katika mambo ya uchawi, nyota, mizimu, kuangalia nyakati mbaya na
mafundisho ya dini za Mashariki ambayo kwa kiwango kikubwa huwanasa
vijana. Kama haya hayatoshi, kuna ongezeko kubwa la viongozi wa kiroho
wanaojiweka wenyewe badala ya kuitwa na Mungu.
Mambo haya yanapingana na maagizo Mungu yanayopatikana katika kitabu cha
Kumbukumbu la torati yanayosema kuwa: “Asionekane kwako mtu
ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu
atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri,
wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye
pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo
ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako,
anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako” (Kumbukumbu
la Torati 18:10-13). Ukengeufu tulioutaja umeenea kama donda ndugu kila mahali katika mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea.
3)Kuanzishwa upya kwa taifa la Israeli
Tayari tumeonyesha umuhimu wa taifa la Israeli katika usitawi na
maendeleo ya wanadamu wote. Kuanzishwa tena kwa taifa hili hakukuwa
tu kwa maana kwa taifa la Israeli, bali ilikuwa pia ni ishara ya kuvutia
inayoashiria kukaribia kwa siku ya kurudi kwa Yesu na ya hukumu ya
mwisho. Zaidi ya miaka 2,500 Mungu alimpa nabii Ezekieli ujumbe ufuatao;
“Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa
walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao
wenyewe; … Katika miaka ya mwisho, utaingia nchi … juu ya milima ya
Israeli, iliyokuwa ukiwa wa daima; … Itakuwa katika siku za mwisho,
nitakuleta upigane na nchi yangu, ili mataifa wanijue” (Ezekieli 37:21;
38:8.16).
Mwaka 1948 ulimwengu kwa mara ya kwanza ulishuhudia kurudi kwa Wayahudi
kwa wingi kutoka katika pande zote za dunia, na kuingia katika nchi yao
iliyofufuka tena. Baada ya kuingia katika nchi yao ilichukua miaka
isiyozidi ishirini, kwa Israeli kuwa taifa mashuhuri lenye nguvu katika
maswala ya kisiasa,kijeshi na kiuchumi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Sawasawa na maneno ya manabii katika Biblia, taifa hili liligeuza eneo
la jangwa kuwa mashamba yenye wingi wa mazao.
4)Kuinuka kwa taifa la Urusi kijeshi
Unabii mwingine unaohusu siku za mwisho uliotimia ni ule ulioandikwa
katika sura ya 38 ya kitabu cha Ezekieli. Maendeleo yaliyofikiwa na
taifa la Urusi na umaarufu wake kijeshi, vinalingana na unabii huu.
Mpaka sasa mataifa ya bara la Ulaya Magharibi na Asia yanamwangalia
“Dubu wa Siberia” kwa tahadhari kubwa. Hii ni kwa sababu, kufuatana na
unabii katika kitabu cha Ezekieli, katika siku siku za mwisho dubu huyu
atatoka katika pango lake, ili kushindana na Simba aliye wa kabila la
Yuda.
5)Kuongezeka kwa maarifa
Kuongezeka kwa maarifa ni jambo lingine tunalokutana nalo katika unabii
wa Danieli unaohusu siku za mwisho. Katika kitabu cha Danieli tunasoma
maneno yafuatayo; “Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya,
ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko
na huko, na maarifa yataongezeka” (Danieli 12:4)
Inavyoonekana siku hizi, maarifa ya wanadamu na elimu vimeongezeka kwa
namna ya kushangaza.Katika karne chache zilizopita
mwanadamu alijishughulisha katika uvumbuzi uliozaa vitu kama ndege,
roketi, simu, televisheni, tovuti, kompyuta, na utandawazi. Ujuzi na
elimu vimeongezeka kiasi cha kuufanya ulimwengu uchanganyikiwe.
Haijawahi kutokea wakati wowote katika historia ya wanadamu ambapo
kumekuwa na ubunifu na uvumbuzi unaoenea kwa kasi kama ilivyotokea
katika siku tulizo nazo.
6)Bomu la Atomu na silaha za Nyuklia
“Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hizo
mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na
kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa
kuwa vitu vyote hivi vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa
tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku
ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa
zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?” (2 Petro
3:10-12). Unabii huu wa mtume Petro wa siku za mwisho na kuja
kwa Bwana unahusishwa na kipindi cha bomu la atomu na silaha za nyuklia.
Kwa ujumla kama mtu yeyote atatafakari kwa kumaanisha maneno
yanayopatikana katika Biblia takatifu, mashaka na kejeli zake dhidi ya
Biblia vitageuka kuwa heshima kuu.
7)Kununua na kuuza kwa kutumia namba
“Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa
maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa
kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote
asiweze kuuza wala kununua, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la
mnyama yule, au hesabu ya jina lake” (Ufunuo 13:16-17).
Maandiko ya aya hizi yanahusu unabii unaohusu kipindi kitakachokuwepo
kabla ya siku ya Mwisho. Kulingana na maandiko haya, unabii huu
unazungumzia kuanzishwa kwa utaratibu kufanya biashara kwa kutumia njia
za kielectroniki badala ya pesa taslimu. Kulingana na mfumo huu, kila
mtu atapewe namba inayomhusu yeye binafsi, inayoendana na jina lake na
asipokuwa na namba hiyo hataweza kununua, wala kuuza kitu chochote. Siku
hizi karibu asilimia themanini hivi za shughuli za kifedha
(transactions) hufanywa kwa njia hizi za kielektronic zinazohusisha
matumizi ya kadi.
8)Kurejea kwa dola ya Rumi
Katika kitabu cha Danieli sura ya 7 na pia katika kitabu cha Yohana,
tunakutana na unabii mwingine unaohusu kuanzishwa tena kwa dola ya Rumi
kabla ya kuwadia kwa Siku ya Mwisho. Wanatheolojia wanahusisha unabii
huu na Jumuiya ya uchumi ya Ulaya, iliyoanzishwa na mataifa machache ya
Ulaya katika mkataba uliotiwa sahihi katika mji wa Rumi. Kuondolewa kwa
mipaka na kuwepo kwa sarafu moja katika mataifa ya jumuiya hii, ni
ishara nyingine inayolenga kuwadia kwa mwisho wa nyakati.
9)Kuanzishwa kwa umoja wa mataifa
Katika kitabu cha mwisho cha Biblia tunasoma juu ya kuanzishwa kwa
utawala wa dunia nzima, utakaotokea wakati wa siku za mwisho. “Nikaona
kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo
lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstajabia mnyama yule.
Wakamsujudia yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao
wakamsujudia yule mnyama, wakasema, Ni nani afananaye na mnyama huyu?
Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? Naye akapewa kinywa cha kunena
maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo kufanya kazi yake miezi
arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana
jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya
vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na
jamaa na lugha na taifa. Na watu wote wakaao juu ya uso wa nchi
watamsujudia, kila mtu ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha
uzima cha mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia” (
Ufunuo 13:3-8). Kuanzishwa kwa umoja wa mataifa (UNO) pamoja na
miundo yake ya kijeshi, uchumi, na shirika la fedha duniani, ni moja ya
dalili ya wazi ya kukaribia kwa siku ya mwisho.
10)Kasi ya kuhubiriwa kwa injili ya Ufalme
Yesu Kristo anasema: “Habari Njema ya ufalme itahubiriwa katika
ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho
utakapokuja” (Mathayo 24:14; Luka 24:47; Matendo 1:8).
Kuhusiana na dalili hii ni wazi kuwa kukua kwa sayansi na tekinolojia
pamoja na kuenea kwa Ukristo, vimechangia kuleta mabadiliko yaliyoupata
ulimwengu katika karine zilizopita. Kuwepo kwa njia za kisasa za
mawasiliano kwa kiwango kikubwa kumechangia kufikiwa kwa maendeleo haya
ya Umisheni wa imani ya Kikristo. Kuenea huku kwa injili ya ufalme wa
Mungu dalili ya wazi inayoonyesha kukaribia kwa siku ya kurudi kwa Yesu.
No comments :
Post a Comment