WASIFU WA MAREHEMU EMMANUEL MAKAIDI KWA UFUPI:
Dk Emmanuel Makaidi
alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD na ni mhandisi aliyebobea.
Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake
mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa la Anglikana.
Alianza elimu
katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 –
1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle school)
iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari
ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne
kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa la 13 na 14
(kidato cha tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati
ya mwaka 1957 – 1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba
yake, la hasha, alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona
anafaulu mitihani yake kwa alama za juu sana.
Makaidi aliendelea
kufadhiliwa na askofu huyo ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na
kumtafutia chuo Afrika ya Kusini. Akapelekwa Chuo Kikuu cha
Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya
mwaka 1958 – 1960.
Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea
kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea
Marekani na kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya
uzamili kati ya mwaka 1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha
Howard kilichoko jijini Washington, Marekani.
Baada ya kurejea
nchini akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966
hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu, katika kitengo cha Utumishi.
Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili). Alirudi tena Marekani na
kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa katika Chuo
Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na mmoja wa maprofesa nguli
duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata tabia ya kuandika
vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na profesa huyu
mahiri.
Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na
kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi nyingine kubwa
zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye kamati iliyokuwa
inashughulikia mashirika ya umma nchini.
Wakati anaendelea na kazi
utumishi, alipata fursa nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata
Taarifa za Kielektoniki katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland.
Alikwenda huko na kuhitimu mwaka huohuo 1977.
Kabla hajafanya kazi
katika kamati maalum ya kusimamia mashirika ya umma akapandishwa cheo na
kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka
huohuo 1985 akafukuzwa kazi.
Kisa cha Makaidi kufukuzwa kazi
serikalini, tena akiwa na wadhifa huo ilikuwa ni kwa sababu ya kuandika
kitabu cha Kiingereza chenye jina “mwanasiasa mwenye roho ya shetani”.
Serikali ikamzonga vilivyo, ikamtuhumu kuwa kitabu kile kinamtukana
Mwalimu Julius Nyerere. Mwisho wa siku “kazi ikaota mbawa”.
Bahati
nzuri, mwaka huohuo 1985 akaajiriwa na Shirika la Finwork Directory kuwa
Mkurugenzi Mtendaji, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1991.
Kuanzia
mwaka 1992 hadi mauti yanamkuta, Dk Makaidi hakujishughulisha tena na
kazi za serikalini wala mashirika binafsi. Alijiajiri akiwa na kampuni
kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya kawaida, lakini pia
aliendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za ndani na nje ya
nchi huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti.
Dk Makaidi alikuwa mwandishi mzuri wa vitabu, alishaandika zaidi ya 10. Amemuacha mjane Modesta Ponela na watoto wanane
No comments :
Post a Comment