Wiki
hii maskio yote ya Watanzania yanaelekezwa mjini Dodoma, mji mkuu wa
Tanzania ambapo chama tawala nchini humo Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kinamchagua mtu mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika
uchaguzi mkuu wa wabunge na rais unaotarajiwa kufanyika tarehe 25 Oktoba
2015.
Vikao vya mchakato huo vinaanza rasmi Jumatano
huku vikitanguliwa na kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo
kimsingi pamoja na mambo mengine kitapitia wasifu wa watia nia wote
lakini pasipo kupunguza jina lolote.
Siku ya Alhamisi (09 Julai),
Kamati Kuu ya chama yenye wanachama takribani 32 itakutana na hapo ndipo
upungazaji wa majina utafanyika hadi kufikia majina matano tu.
Baada
ya hapo, Halmashauri kuu ya chama itakutana siku ya Ijumaa tarehe 10
Julai ambapo itachuja majina hayo matano hadi kufikia matatu kupitia
mtindo wa kupiga kura. Majina haya matatu ndiyo yatakayokwenda katika
Mkutano Mkuu wa Chama ambao ndio utakaochagua jina moja la huyo mgombea
urais kwa tiketi ya chama
Mkutano Mkuu huu unajumisha takribani
wanachama 2100 ikiwa ni pamoja na Wabunge wa CCM Tanzania bara na
wawakilishi wengine kutoka Zanzibar lakini pia wawakilishi wa chama
kutoka ngazi mbalimbali hadi zile za chini.
Mkutano huu umepangwa kufanyika tarehe 11 hadi 12 Julai
Uteuzi waibua hisia Tanzania
Wakati
watu wakingojea kwa hamu ni nani atapenya katika mchujo huo na kuibuka
kidedea, tangu mwanzo wa zoezi zima la kutafuta nafasi hiyo kwa
wanachama wa CCM kumeibua hisia kubwa na za tofauti miongoni mwa
Watanzania.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya CCM na nchi kwa
ujumla, idadi ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu na kusaka ridhaa
ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho ilifikia 42.
Idadi
hii ilijumuisha makada kutoka kila aina ya haiba. Walikuwemo waliokuwa
mawaziri wakuu wa zamani, maofisa wa ukachero wastaafu na hata
mwanachama mmoja ambaye elimu yake inasemekana kuwa ni ya shule ya
msingi tu. Hata hivyo orodha hii ilisheheni jinsia ya kiume zaidi huku
idadi ya wanawake waliojitokeza kuchukua fomu ikiwa ni wane tu.
Mchakato huu wa CCM kuelekea
uteuzi wa mgombea wao wa urais ni wa muhimu sana kwa chama hicho na
unafuatiliwa kwa karibu sana na wapenzi lakini hata wapinzani wa chama
hicho kwa sababu mwisho wake unatarajiwa kutoa picha ya mwelekeo wa
chama hicho kikongwe nchini.
Umuhimu wa mchakato
Kwa
mfano, huu ndio msimu wa kwanza ambapo chama hicho kitamteua mgombea
urais pasipo baraka za moja kwa moja za mwasisi wa chama hicho na taifa
kwa ujumla Mwalimu Julius Nyerere.
Hata kama vyombo husika vya
uchaguzi na utaratibu mzima wa kumpata mgombea umekuwepo tangu kitambo,
Mwalimu Nyerere alifanyika mshawishi mkubwa katika kuwapata wagombea
hasa wa nafasi nyeti kama ya urais wa nchi ambao hatimaye kweli walipata
kuwa marais.
Kwa upande mwingine baadhi ya wanaosaka kuteuliwa
kuwa wagombea wa chama chama hicho wamehusishwa na kashfa kadhaa za
matumizi mabaya ya madaraka na rushwa vilivyoisababishia serikali hasara
kubwa na kuzua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania
CCM
inaonekana kuwa na kazi ngumu ya kuwahakikishia wanachama wake lakini
pia wapinzani wake kwamba ina uwezo wa kumuweka kando mtuhumiwa yeyote
kwa usalama wa chama. Kwamaneno mengine, kuthibitisha kwamba chama
ndicho kinachotangulia halafu mgombea anafuata.
Lakini wakati CCM
inapiga hesabu ya kuruka kihunzi hicho, bila shaka inapiga hesabu
nyingine pia ya namna gani itahakikisha chama kinabaki imara hata baada
ya kuwanyima fursa hiyo wanachama hawa wanaonekana kuwa na madoa
Ikumbukwe
kwamba hao wanaoshutumiwa ni makada wenye ushawishi wa hali ya juu na
wafuasi wengi ndani ya chama ambao bila shaka wanauwezo wa kuhatarisha
umoja na uhai wa chama ikiwa wagombea wao watanyimwa fursa hiyo.
Mwaka
jana CCM ilionesha makeke yake baada ya kuwasimamisha makada wake sita
kwa muda wa takribani miezi 17 ambao walibainika kukiuka kanuni za
uchaguzi cha chama.
Ni nani ataaminiwa kupewa dhamana ya
kupeperusha bendera ya CCM? Na ni nini mustakabali wa chama hicho baada
ya mchakato wa kumpata mgombea huyu wa tiketi ya chama? Maswala haya na
mengine mengi bila shaka yapata majibu yake baada ya kikao cha chama
hicho.
No comments :
Post a Comment