John Pombe Magufuli mgombea urais CCM
Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania John Pombe Magufuli amechaguliwa kupeperusha bendera ya chama tawala CCM wakati wa uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Magufuli mwenye umri wa miaka 55, alimshinda Asha-Rose Migiro ambaye ni
Waziri wa Katiba na Sheria na Amina Salum Ali, Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Tume ya Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa nchini
Marekani.
Wawili hao walifika katika hatua ya tatu bora na kupigiwa kura siku
ya Jumamosi usiku na baadaye matokeo yakatangazwa siku ya Jumapili.
Akitangaza matokeo hayo, Spika wa bunge Anna Makinda alisema
Magufuli alipata ushindi wa kura za wajumbe 2,104 sawa na asilimia
87.1, akifuatwa na Amina Salum Ali aliyepata kura 253 sawa na asilimia
10 nukta 5 huku Asha Migoro akimaliza wa tatu kwa kupata kura 59 sawa
na asilimia 2 nukta 4.
Kwa ushindi huu, Magufuli ndiye atakayemenyana na mgombea wa upinzani
na ikiwa atashinda atakuwa rais wa tano wa Tanzania baada ya rais
Jakaya Kikwete.
Magufuli anayefahamika kwa umaarufu wake wa kutaja takwimu za
Kilomita za barabara zilizotiwa lami, amewaambia wajumbe wa CCM kuwa
atahakikisha kuwa anakiunganisha chama hicho na kufanya kampeni
kuhakikisha kuwa chama hicho kinapata ushindi tarehe 25 mwezi Oktoba.
Wanasiasa 38 wa CCM waliomba nafasi ya kupeperusha Bendera ya chama
hicho akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowasa na Waziri wa Mambo ya
nje Bernard Membe.
Siku ya Jumamosi kulikuwa na hali ya wasiwasi baada ya kuondolewa kwa
jina la Lowassa ambaye alionekana kuwa na uungwaji mkono wa wananchi
wengi, huku mpinzani wake Bernard Membe akifuzu kuwa katika tano bora.
Baada ya mshindi kupatikana, wajumbe waliohudhuria mkutano huo
walionekana kuzungumza kwa sauti moja na kumuunga mkono Magufuli na
kumpa jina “Jembe” litakalofanya kazi bila kuchoka.
Katika historia ya chama hicho, wanawake wawili walifika katika hatua
ya mwisho huku waliojitokeza kuomba kupeperusha bendera ya chama hicho
wakijitokeza kwa wingi.
Chama cha Mapinduzi ambacho kimekuwa kikiongoza nchi hiyo toka mwaka 1977 kimekuwa kikishinda uchaguzi nchini humo .
No comments :
Post a Comment