Dkt. Bilal awaongoza waombolezaji kuaga mwili wa Marehemu Dkt. Kigoda jijini DSM.
Makamu
wa rais Dk Mohamed Gharib Bilal ameongoza waombolezaji kuuaga mwili wa
aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara Dr.Abdalah Kigoda kabla ya
kusafirishwa kuelekea Handeni mkoani Tanga kwa maziko.
Zoezi hilo limefanyika katika viwanja vya Karemjee jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikali
wakiwemo marais wastaafu Alhaji Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa,
spika wa bunge mama Anne Makinda na katibu mkuu kiongozi balozi Ombeni
Sefue.
Akitoa salaam za serikali waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh
Mathias Chikawe mbali na kuelezea namna marehemu Kigoda alivyolitumikia
taifa kwa uadilifu katika nafasi zote alizopewa au kuteuliwa amesema
wananchi wa jimbo lake la Handeni wamepoteza kiongozi shupavu.
Baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu ambao aliwahi kufanya nao kazi
nao wamepata fursa ya kuelezea utendaji wake ambao wamedai kuwa ulikuwa
shirikishi jambo ambalo ni nadra kwa baadhi ya viongozi.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya sekta binafsi TPSF Bw Godfrey
Simbeye ni miongoni mwa viongozi wa taasisi zilizohudhuria zoezi hilo
ambapo amesema kwa niaba ya TPSF wamtaka rais ajaye na serikali ijayo
kuhakikisha inateua waziri wa viwanda na biashara atakayefuata nyayo za
marehemu Kigoda ambaye alipenda kujadiliana na sekta binafsi.
Marehemu Kigoda alizaliwa Novemba 25 mwaka 1953 wilayani Korogwe
mkoani Tanga na kufariki dunia Octoba 12 mwaka huu huko nchini india
alikokuwa akipatiwa matibabu na ameacha mjane watoto watatu na wajukuu
wanne.
No comments :
Post a Comment